Majeruhi wa ajali ya Basi dogo la abiria, ‘Daladala’ wameelezea jinsi walivyopata majeraha baada ya gari hilo kugonga Lori na kuanguka hapo jana Novemba 22, 2022 katika eneo la Mbezi njia Panda ya kuelekea Goba, majira ya asubuhi.
Majeruhi hao wamesema, ajali hiyo ilitokea baada ya gari hilo kufeli breki wakati linatokea Goba kwenda Kawe na kwamba awali Dereva wao alijitahidi kupambana lakini mteremko wa kutokea Masana ulikuwa mkali na alipofika njia panda aligonga lori ubavuni kisha kupinduka.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi amesema katika ajali hiyo watu tisa wengi wao wakiwa ni wanafunzi walijeruhiwa.
Amesema, gari hilo aina ya Coster lenye namba za usajili T186 DMQ linalofanya safari zake kati ya Mbezi na Kawe, lililokuwa likiendeshwa na dereva Venance Silvester (44), mkazi wa Tegeta.
Kamanda Kitinkwi amesema, “Kabla ya kuanguka gari hilo pia liligonga gari lingine Scania lililokuwa likiendeshwa na Bakhar Barhan (43) lililokuwa linatoka Tegeta kwenda Mwenge.”
Baadhi ya mashuhuda watukio hilo wamesema, Daladala hilo lilipita kwa kasi eneo la makutano ya barabara iendayo tegeta kutokea Goba, na kwamba kasi yake ilizidi kufuatia kuruka tuta la badabarani na ndipo ajali hiyo ikatokea na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.