Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Meja Mstaafu, Abdul Mingange, amesema soka lililochezwa juzi Jumatatu (Juni 19) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, ndilo litakalokwenda kuchezwa Uwanja wa Sokoine Mbeya, kesho Alhamis (Juni 22).
Mchezo huo wa ‘Play Off’ Mkondo wa Kwanza ulishuhudia Mashujaa FC ikiichapa Mbeya City mabao 3-1, mabao yakifungwa na Abiud Mtambuka dakika ya 24, Asanga Stalon (dk. 69) na Shadrack Ntabindi (dk. 78) kwa mkwaju wa penati wakati goli la kufutia machozi la Mbeya City likiwa ni la kujifunga kupitia kwa Aziz Sibo dakika ya 63.
Kocha Mingange amesema dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanacheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, hivyo wanakwenda Mbeya kucheza kwa kujiamini.
Amesema dhamira nyingine ya timu hiyo na wakazi wa Kigoma, ni kuhakikisha wanacheza kwa ari kubwa ndani ya dakika 90 zilizosalia, huku akiwasisitiza Mashabiki kuwaombea ili wafanikishe lengo wanalolikususdia.
“Tulistahili kushinda kuna watu wana wasiwasi kuwa labda tutakwenda kupoteza Mbeya kwa sababu mechi ya kwanza ya ‘Play Off dhidi ya Pamba tulishinda na mabao 4-0, lakini tukaenda kuruhusu mabao 4-1, bao moja la ugenini likatuvusha, lakini kwa hili nawahakikishia tunakwenda kuwashangaza huko huko kwao, hii timu yangu ina uwezo wa kupata bao ugenini, tukifanikiwa kufunga tu huko bao moja au zaidi, tayari ndoto zetu zitakuwa zimetimia,” amesema Mingange ambaye alikuwa akiifundisha pia timu ya Mbeya City, na Ndanda FC.
Mashujaa iliyokuwa Ligi ya Championship, ilifanikiwa kufika hatua hiyo baada ya kuiondoa Pamba kwenye mechi ya mchujo kwa jumla ya mabao 5-4, sasa inatakiwa kushinda, kupata sare au kufungwa bao lisilozidi moja ili kupanda Ligi Kuu, ikiifuata JKT Tanzania na Kitayosce ambayo kwa sasa imebadilishwa jina na kuitwa Tabora United.
Kwa upande wa Mbeya City, hii ni mara ya pili kucheza ‘Play Off’, msimu wa 2019/20 ilicheza dhidi ya Geita Gold wakati huo ikiwa Championship, lakini ilifanikiwa kubaki kwa jumla ya mabao 2-1, kwa sare ya bao 1-1 ugenini na kushinda 1-0 nyumbani, Mbeya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, aliahidi kutoa usafiri kwa mashabiki wa soka mkoani humo kwenda jijini Mbeya kuipa hamasa na kuishangilia Mashujaa FC, baada ya kufurahishwa na ushindi, lakini umati uliojitokeza na kushangilia kwa aina yake.