Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mataifa Ulimwenguni kutambua umuhimu kuweka mkazo katika taasisi ya familia ya kiutamaduni, ili kuifanya kuwa kiini cha maendeleo ulimwenguni.
Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati akihutubia kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tano wa Idadi ya Watu (5 th Budapest Demographic Summit) unaofanyika Jijini Budapest nchini Hungary na wito kwa serikali ulimwenguni kutengeneza na kutekeleza sera, programu na sheria zitakazohakikisha usalama na uendelevu wa familia.
Amesema, inahitajika nguvu ya pamoja kimataifa katika kuimarisha ustawi wa familia ikiwemo kuzingatia kanuni na desturi za kiutamaduni pamoja na kuunga mkono mafundisho ya dini ambayo yanakuza maadili ya familia na kulinda usalama na mwendelezo wa familia.
Aidha, Dkt. Mpango ameongeza kuwa Bra la Afrika linahitaji kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko la idadi ya watu na uhitaji wa huduma za afya na elimu, ukosefu wa ajira, upungufu wa chakula na uhamiaji haramu.