Kocha Mkuu wa muda wa Simba SC Seleman Matola amesema haikuwa rahisi kwa kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City FC jana Alhamis (Juni 16), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mabao ya Simba SC katika mchezo huo yalifungwa na Kiungo Mshambuliaji kutoka Senegal Pape Ousman Sakho aliyefunga mawili na Peter Banda kutoka Malawi.
Matola ambaye alikabidhiwa kikosi cha Simba SC baada ya kuondoka kwa Kocha Franco Pablo Martin mwezi uliopita, amesema Mbeya City ilicheza vizuri na imekua kawaida yao kufanya hivyo inapokutana na timu yake.
Amesema ilimlazimu kubuni mbinu za kuipangua safu ya ulinzi ya Mbeya City uliyokua na watu wengi zaidi, na ndipo mambo yalipomnyookea na kuiwezesha timu yake kuondoka na alama tatu.
“Siku zote tukicheza na Mbeya City huwa tunapata changamoto kubwa sana ya ushindani, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata ushindi huu, haikuwa raisi, kwa sababu wapinzani wetu walikuja na mfumo wa kuzuia na kucheza kwa kasi ya chini,”
“Ilinilazimu kama Kocha kupanga mbinu za kuivunja safu yao ya Ulinzi iliyokua na watu wengi ili kupata ushindi, tumefanikiwa katika hilo na tunaondoka katika uwanja wa nyumbani tukiwa tumekamilisha mpango wetu wa ushindi.” Amesema Matola
Ushindi huo umeiwezesha Simba SC kufikisha alama 54 zinaoendelea kuiweka nafasi ya pili kwenye msimamo, huku Young Africans aliyojitangazia ubingwa juzi Jumatano (Juni 15), ikiwa kileleni kwa kuwa na alama 67.
Simba SC itarudi tena dimbani juma lijalo (Alhamis-Juni 23) kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar kutoka mkoani Morogoro, katika Uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.