Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Seleman Matola, amewatuliza Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kwa kuwaambia matokeo ya mchezo wa jana Jumanne (Septamba 28) yasiwakatishe tamaa, kwani bado shughuli ni kubwa na wataimaliza kwa kutetea taji lao msimu huu 2021/22.
Simba SC ilicheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22 dhidi ya Biashara United Mara na kuambualia sare ya 0-0, katika Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
Matokeo hayo hayo yameibua hisia tofauti kwa baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kwa kuamini kikosi chao kimeporomoka kiwango na huenda msimu huu mambo yakawa magumu katika kuuendelea ubingwa wa Tanzania Bara.
Matola amesema hakuna haja kwa Mashabiki na Wanachama kuingiwa simanzi kwa kilichojitokeza jana Jumanne, na badala yake amewahimiza kuendelea kukiamini kikosi chao kuelekea mchezo unaofuata dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Amesema mchezo wa jana haikuwa bahati kwa Simba SC kuibuka na ushindi, lakini kwa ujumla wachezaji walipambana na walionesha kuwa na uchungu kwa kushindwa kupata matokeo.
“Haikuwa bahati yetu, wachezaji walipambana kwa namna ambavyo wanaweza lakini tumeshindwa kushinda, matokeo tunayachukua tutafanya kazi mchezo ujao kwani ligi inaanza na kila timu inahitaji ushindi.” amesema Matola.
Taharuki kwa baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Simba SC imeongezeka baada ya kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Jumamosi (Septamba 25), dhidi ya Young Africans iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0.
Simba SC itakua ugenini kwa mara ya pili mfululizo, Jumamosi (Oktoba 02) mjini Dodoma kwenye Uwanja wa CCM Jamhuri kwa kucheza dhidi ya Dodoma Jiji FC, ambao wameanza vizuri kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting jana Jumanne (Septemba 28).