Kitendo cha baadhi ya wazazi na walezi kutosimamia nafasi katika malezi ya watoto, kumekuwa kukichangia mmomonyoko wa maadili na kukithiri kwa vitendo vya kikatili katika jamii hasa kwa watoto.
Mkuu wa dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Mrakibu wa Polisi, Asia Matauka ameyasema hayo wakati wa mkutano wa maadhimisho ya siku ya Familia, uliofanyika soko la Pasua lililopo mjini Moshi.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa na matukio ya ukatili yanayoendelea kukithiri ambayo yanawaathiri watoto wengi hasa ubakaji na ulawiti, na kuitaka jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja ili kudhibiti hali hiyo.
“Kwa mwezi Aprili mwaka huu (2023), tumepokea kesi zaidi ya 20 za matukio ya ubakaji na ulawiti, vitendo vya ubakaji na ulawiti mkoani Kilimanjaro vinakithiri lakini pia usagaji na Ushoga upo hii yote inatokana na mmomonyoko wa maadili na kukosa hofu ya Mungu,” amesema Matauka.
Awali, Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Moshi, Lulu Siame alisema wazazi wengi wamesahau jukumu lao la malezi ya watoto na wengine wakihofia kuwakemea na kuwaonya wakati wanapoenda kinyume cha maadili kutokana na hofu.