Mchungaji Eliud Wekesa, maarufu kama Yesu wa Tongaren raia wa Magharibi mwa Kenya, amejisalimisha kwa maofisa wa Polisi kwa mahojiano baada ya kutakiwa kufanya hivyo ikiwa ni hatua mojawapo ya Serikali ya kuwadhibiti wahubiri wenye misimamo na itikadi kali.
Wekesa ambaye ni kiongozi wa dhehebu la New Jerusalema anayejitangaza kuwa yeye ndiye Yesu na kwamba ana malaika wake ambao wanamsaidia katika kazi yake kama kristo mwana wa Mungu alitakiwa na Polisi kwa mahojiano juu ya mafundisho yake ya kidini yanayotiliwa shaka.
Katika kujinasibu, Wekesa pia hudai ana wanafunzi kumi na wawili kama ilivyokuwa katika Bibilia na wakati wa Yesu Kristo mwana wa Mungu na amekuwa akisisitiza kwamba yeye anafanya kazi ya kueneza injili kwa viumbe waliopotea.
Hatua ya kutakiwa kufika mbele ya polisi kwa kiongoizi huyo wa dini inakuja wakati huu maofisa wa usalama katika eneo la pwani ya Kenya wakiwa wanaendelea na zoezi la kufukua miili zaidi ya watu wanaodhaniwa kuwa walizikiwa baada ya kufairiki wakifunga kula kama walivyotakiwa na mhubiri wao Paul Makenzie.