Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Makao Makuu imewaita wabunge wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na waliowahi kuwa wabunge wa chama hicho kwaajili ya mahojiano.
Taarifa iliyotolewa na Taasisi hiyo kupitia kwa afisa uhusiano, Doreen Kapwani, imeeleza kuwa hatua hiyo inafanyika ikiwa ni mwendelezo wa uchunguzi unaoendeshwa juu ya malalamiko dhidi ya matumizi ya fedha za CHADEMA ambapo hatua iliyopo sasa ni kuwahoji wabunge 69, wanachama na waliowahi kuwa wanachama wa chama hicho.
Imeelezwa kuwa fedha hizo ni zile ambazo zililalamikiwa na waliokuwa wabunge wa CHADEMA ambapo katika malalamiko yao walidai kwamba walikuwa wakikatwa fedha katika mishahara yao kila mwezi kuanzia mwezi juni 2016.
Kwa mujibu wa malalamiko hayo, kila mwezi wabunge wa viti maalum walikuwa wakikatwa kiasi cha shilingi 1,560,000 na wabunge wa kuchaguliwa kwenye majimbo walikuwa wakikatwa shilingi 520,000 na hawakuwa wakifahamu namna ambavyo fedha hizo zimekuwa zikitumika.
TAKUKURU imesema kutokana na tuhuma hizo kunaweza kupatikana makosa mawili; Ubadhirifu na ufujaji wa fedha za chama na Matumizi mabaya ya mamlaka.
Makosa yote hayo yanaangukia katika sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Aidha imeelezwa kuwa hadi sasa viongozi ambao tayari wamehojiwa ni, Viongozi wa CHADEMA, viongozi waliowahi kuwa CHADEMA, Wabunge waliotoa taarifa, Maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Viongozi wa bodi ya wadhamini CHADEMA pamoja na wabunge.