Waziri wa mambo ya ndani wa Pakistan, Ran Sanaullah amesema ushahidi uliopo unaonyesha kuwa Mwandishi wa Habari maarufu raia wa nchi hiyo, Arshad Sharif aliuawa kwa mauaji ya kupanga nchini Kenya, na kwamba kifo chake hakikutokana na ufyatuaji risasi kimakosa.
Arshad Sharif aliuawa kwa bunduki jioni ya Oktoba 23 jijini Nairobi, ambapo ripoti ya Jeshi la Polisi wa Kenya ilieleza kuwa askari waliokuwa wakifanya msako kutafuta wezi wa magari, walilifyatulia risasi gari aliyokuwa akisafiria mwandishi huyo kimakosa.
Ripoti hiyo, ilizidi kueleza kuwa kitendo cha kufyatua risasi kilitokana na gari alilokuwa akisafiria mwandishi huyo kupita katika kizuizi cha barabarani bila kusimama, ishara ambayo walidhani ni moja kati ya magari yaliyokuwa yakihisiwa kuwa ni la uhalifu.
Hata hivyo, Taasisi ya kufuatilia maadili ya Polisi wa Kenya imesema inachunguza kisa hicho huku Waziri huyo wa mambo ya ndani wa Pakistan akisema ushahidi walioupata unaonyesha kuwa yalikuwa mauaji ya kupanga, na wanaendelea kukusanya taarifa zaidi kwa ushirikiano na Kenya.