Simulizi ya kijana Majaliwa Jackson, aliyehusika kuwaokoa Watu 24 kwenye ajali ya ndege iliyotokea Bukoba Novemba 6, 2022.

Majaliwa anasema, “Niliingiwa na hofu nilipoona ndege hiyo ya abiria ikielekea upande usiofaa, kabla ya kutumbukia ziwani na nilikimbia hadi eneo la tukio tukiwa na wavuvi wenzangu watatu na kusaidia kufungua mlango wa nyuma kwa kuuvunja kwa kasia iliyowasaidia abiria waliokuwa wameketi nyuma ya ndege kuokolewa.”

Ameongeza kuwa, “Kisha nikasogea mbele na kuzama majini. Kisha Mimi na mmoja wa marubani tuliwasiliana kwa ishara kupitia dirisha la chumba cha marubani ambaye alinielekeza nivunje kioo cha dirisha, nilitoka majini na kuwauliza wanausalama wa uwanja wa ndege ambao walikuwa wamefika kama wana vifaa ambavyo tunaweza kutumia kuvunja kioo.”

Kijana Majaliwa Jackson.

Majaliwa ameendelea kusimulia kuwa, “Walinipa shoka, lakini nilizuiwa na mtu ambaye ni mhudumu wa uwanja, aliyekuwa na speaker akisema tayari Wana mawasiliano na marubani na hakuna maji yanayoingia kwa haraka kwenye chumba cha rubani.”

Anasema, “Hata hivyo mimi nilikuwa naona maji yakiingia kwa wingi kwenye ndege na baada ya kusimamishwa, niliwaonea huruma marubani, nikawapungia mkono wa kwaheri kuwaaga marubani lakini yule Rubani bado alionyesha kwamba alitaka kuokolewa.”

Mmoja wa abiria ambae alinusurika katika ajali hiyo ya Ndege, Nikson Jackson, kushoto ni miili ya Wafanyakazi watano wa Shirika la Management and Development for Health (MDH), waliofariki katika ajali hiyo.

Aidha, Majaliwa anabainisha kuwa, “Rubani alininyooshea kwa ishara mlango wa dharura wa chumba cha marubani, nikaogelea nyuma na kuchukua kamba na kuifunga mlangoni na tukajaribu kuivuta kwa boti nyingine lakini kamba hiyo ilikatika na kunipiga usoni nikapoteza fahamu na sikujua kitu hadi nilipojikuta nipo hapa hospitalini.”

Hiyo ni simulizi ya Majaliwa Jackson kuhusu nia yake ya kuwaokoa marubani, Majaliwa alizawadiwa shilingi milioni moja na wa Waziri Mkuu na baadaye Rais Samia alimpigia Waziri Mkuu na kuagiza Majaliwa apewe mafunzo maalum kwenye jeshi la uokozi na kiisha aajiriwe jambo ambalo tayari limeanza utekelezaji.

Oppa Clement atajwa kikosi bora Afrika
Mauaji ya Mwandishi Kenya yalipangwa: Waziri