Aliyekuwa Meneja wa muda wa Chelsea, Frank Lampard amemuonya Meneja mpya Mauricio Pochettino kwamba haitakuwa kazi rahisi kupindua meza baada ya kuteuliwa kukinoa kikosi hicho kuanzia msimu ujao.
Vilevile Lampard ameponda kiwango cha Chelsea baada ya kumaliza ligi nafasi ya 12 kwenye msimamo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 1995-1996.
The Blues ilimaliza katika nafasi hiyo kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Newcastle United na mara ya mwisho iliweka rekodi mbovu zaidi msimu wa 1993-1994 kwani ilimaliza nafasi ya 14.
Lampard ambaye alirejea Chelsea kama Meneja wa muda baada ya Graham Potter kufukuzwa kazi Aprili, alikichambua kikosi akidai kazi kubwa inahitajika.
“Ubora wa Chelsea umeporomoka kwa kiasi kikubwa, naongea ukweli kabisa, naweza nisionane na baadhi ya wachezaji baada ya hapa kwa sababu nyingi tu,” amesema Lampard
“Chelsea haikuwa na ushindani kabisa, haikucheza soka la kiwango cha juu, nilipokuja hapa nilitambua tu mambo sio shwari, bila shaka hata kocha mzuri akitokea anaweza kusaidia lakini wachezaji pia wanatakia kuwajibika asilimia 100, benchi la ufundi na mabosi kwa ujumla”
Baada ya Pochettino kusaini mkataba kufuatia mazungumzo yaliyodumu majuma kadhaa, Lampard alimuonya kazi itakuwa ngumu kwa sasabu mambo ya kubadilisha timu yatakuwa makubwa.
“Mimi ni shabiki wa Pochettino, lakini itachukua muda mrefu hadi kufikia mbali Chelsea kwa hiyo haitakuwa rahisi.” Amesema Lampard