Kocha Mkuu wa Chelsea, Mauricio Pochettino ameripotiwa kuwa na mpango wa kufanya usajili wa mastaa wasiopungua watatu kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa Januari, 2024.
Wakati The Blues ikiwa bado haijapata kasi yake tangu kocha huyo kutoka nchini Argentina alipotua Stamford Bridge, timu hiyo kwa sasa inashika namba 12 kwenye Ligi Kuu.
Kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Everton cha Jumapili (Desemba 10), kiliifanya Chelsea kupoteza mechi tatu kati ya nne za mwisho, huku vichapo vingine vikitoka kwa Newcastle United na Manchester United na hivyo The Blues kwa sasa ipo nyuma kwa pointi 14 kuifikia Manchester City iliyopo kwenye Top Four.
Baada ya kipigo cha Goodison Park, Pochettino amesema kikosi chake kinahitaji sura mpya za kuja kuongeza nguvu kwenye dirisha la Januari 2024, licha ya Chelsea kutumia zaidi ya Pauni 1 Bilioni kwenye usajili wa madirisha matatu yaliyopita.
Kocha Pochettino wala hajali hilo na kutaka mabosi wa timu hiyo kufanya usajili wa mastaa watatu wakati dirisha litakapofunguliwa.
Pochettino ameweka wazi kwamba anahitaji beki wa kati, kiungo wa kati na Mshambuliaji waje kuongeza nguvu na kuboresha ubora wa kikosi chake.
Licha ya Chelsea kufunga mabao 26 katika mechi l6 kwenye Ligi Kuu England msimu huu, bado kiwango chake cha kufunga si bora sana, huku Mshambuliaji wao Nicolas Jackson bado anajitafuta, hajaonyesha makali yake tangu alipotua kutoka Villarreal.
Mshambuliaji Armando Broja anarejea kwenye kikosi taratibu akitokea kwenye majeruhi, huku Christopher Nkunku akiwa hajacheza mechi yoyote kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, hivyo Chelsea inakosa nguvu kwenye eneo lake la ushambuliaji.
Pochettino amedai kimo pia kimemfanya awatumie wachezaji Axel Disasi na Levi Colwill kwenye beki za pembeni badala ya kati.