Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini (CCM), Anthony Mavunde amesema kuwa asilimia kubwa ya akina mama wajawazito wanapata tabu wakati wa kujifungua kwa kukosa vifaa muhimu .

Ameyasema hayo jijini Dodoma katika kituo cha afya cha Makole, wakati akikabidhi misaada katika kituo hicho ikiwa ni kuonyesha upendo kwa mama wajawazito wanao kwenda kujifungua ikiwa ni siku ya wapendanao.

Amesema kuwa siku ya tarehe 14/2 ni siku ambayo watu wengi wamekuwa wakiitafsiri tofauti lakini kwa upande wake anaamini kwamba upendo ni kuwajali watu wenye mahitaji, hivyo aliamua kutoa msaada huo ili kuweza kuwasaidia kina mama hao.

”Nimeamua kuleta dawa zitakazosaidia wakati wa uchungu, kama alivyosema Daktari lakini pia nimeongeza na haya mashuka yenye thamani ya zaidi ya milioni moja na vitu hivi vitasambazwa katika vituo vya afya tofauti tofauti na ninayafanya haya sio kama ninauwezo hapana, ila tu ni wajibu wetu viongozi katika kutatua kero za wananchi,”amesema Mavunde

Aidha, katika hatua nyingine, Mavunde amesema kuwa wakati anaenda kuwaomba ridhaa wananchi mwaka 2015 yako mambo ambayo aliyatamka ikiwemo kusaidia sekta ya afya, ili wananchi wa jimbo la Dodoma mjini wapate huduma salama.

Kwa upande wake Dkt. George Matiko ambaye ni Mganga mfawidhi wa kituo cha Makole amempongeza Mbunge huyo kwa kile alichokifanya kwani si wote wanaofanya kazi kama anayofanya yeye.

 

Mama yake Godzilla ataka nyimbo za injili za mwanaye zichezwe msibani
Wizara ya Afya yatoa msaada wa Kisaikolojia mkoani Njombe