Saa chache kabla ya Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, jijini Dar es Salaam kujibu kesi ya kuhusishwa na dawa za kulevya, wanasheria wake wamewasilisha ombi la kubadili kesi ya kusikilizwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka mahakamani hapo, mawakili wa Manji wanaiomba Mahakama kubadili na kusikiliza kesi ya uhamiaji leo badala ya dawa za kulevya.
Katika kesi ya uhamiaji, wanasheria hao wameeleza kuwa mteja wao anakabiliwa na tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria.
Manji anakabiliwa na kesi ya kujihusisha na dawa za kulevya baada ya kuitwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha yake ya awali ya watuhumiwa iliyopelekea mfanyabiashara huyo kupimwa na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Taarifa zinaeleza kuwa katika kesi nyingine, Mwenyekiti huyo wa Yanga anadaiwa kuwa na hati mbili za uraia, moja ikiwa ya uraia wa Tanzania na nyingine ya uraia wa Uingereza.
Manji anapanda leo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akitokea katika hospitali ya Aga Khan alikolazwa akiwa chini ya ulinzi wa Maofisa wa Uhamiaji na Jeshi la Polisi.
Wanasheria wake wamechukua uamuzi wa kuwasilisha ombi hilo kwani tangu mteja wao alipotuhumiwa na kufunguliwa kesi kwa kosa la kuvunja sheria ya uhamiaji, hakuwahi kupandishwa mahakamani.