Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Maxi Nzengeli, ametoboa siri kwamba, ana uwezo kucheza nafasi yoyote ambayo kocha wake ataamua kumpanga, lakini anafurahi zaidi akicheza kama kiungo.
Nyota huyo tangu atue katika klabu ya Young Africans Julai mwaka huu, amekuwa akiacha maswali mengi kwa mashabiki wa soka kuwa anacheza nafasi gani kutokana na kufiti kila nafasi.
Akizungumza na mtandao wa Young Africans, Nzengeli amesema anacheza nafasi yotote ambayo kocha ataamua kumpanga.
“Nakaba na kushambulia ni sawa nikicheza winga au kiungo, lakini nikipangwa kama kiungo mkabaji nafurahi zaidi kuliko nafasi nyingine,” amesema.
Nyota huyo aliyejiunga na Young Africans akitokea klabu ya Maniema ya kwao DRC, anasema anapokuwa uwanjani anapenda sana kutoa “assist’ na sio kufunga mabao.
“Nafurahi sana nikitoa ‘assist’ na yule ninayempa akifunga bao nafurahi zaidi kuliko nikifunga mimi,” amesema nyota huyo ambaye anapenda kucheza mpira akiwa amechomekea.
Nzengeli amepachika mabao mawili katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara, ambayo timu hiyo imecheza dhidi ya KMC na JKT Tanzania.
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), limeigomea klabu ya E-Merreikh ya Sudan kuhama Uwanja katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya ya Ligi Mabingwa Afrika (CAFCL) dhidi ya Young Africans.
Mchezo huo utachezwa Septemba 16, mwaka huu katika Uwanja wa Kigali Pele nchini Rwanda, ambao El-Merreikh wameutumia katika mchezo wa awali.
El-Merreikh walipanga kwenda kucheza mchezo huo nchini Morocco, lakini umerudishwa nchini Rwanda.