Kikosi cha Young Africans leo Ijumaa (Septemba 14) kimefanya mazoeiz yake ya mwisho mjini Kigali-Rwanda kabla ya kuivaa Al Merreikh ya Sudan katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wakati kikosi cha Mabingwa hao wa Tanzania Bara kikikamilisha maandalizi hayo, kuna kauli imetolewa na kiungo fundi wa timu hiyo, aliyesema huko Kigali moto utawaka kwani wamejipanga kushinda ugenini.
Kiungo aliyetoa kauli hiyo ni Maxi Nzengeli ambaye juzi tu ametoka kubeba tuzo ya kwanza ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu kwa mwezi Agosti ambapo amesema mzuka wa tuzo hiyo utaanzia kwenye mchezo huo utakapoigwa Uwanja wa Kigali Pele (zamani Nyamirambo), jijini Kigali kuanzia saa 10.00 jioni.
Maxi amesema wanakwenda Kigali kufanya jambo moja tu kuhakikisha kikosi kinalainisha safari yao ya kwenda makundi kwa kuichapa Merreikh.
“Kwanza nimefurahia kupata hii tuzo yangu ya kwanza hapa Tanzania hii ni heshima kubwa kwa klabu yangu, wachezaji wenzangu, makocha, viongozi na hata mashabiki wetu wazuri,” amesema Maxi mwenye mabao manne katika mechi za mashindano, yakiwamo mawili ya Ligi Kuu na mengine ya Ligi ya Mabingwa.
“Hii inanipa nguvu ya kunifanya nijitume zaidi, tumekuja Rwanda kucheza mechi ngumu ambayo malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda huko huko. Hesabu zetu ni kushinda kule ugenini ili tukirudi hapa tumalizie kazi kuipeleka timu yetu hatua ya makundi kila mchezaji anatamani hii mechi. ameongeza nyota huyo mwenye asisti moja katika ligi akilingana na Stephane Aziz Ki na Prince Dube wa Azam FC Maxi.
Pia amefichua namna wachezaji wa Young Africans walivyo na mzuka kwa ajili ya mchezo huo, licha ya kwamba utakuwa wa kwanza kwao ugenini tangu msimu huu uanze, kwa vile mechi zote za CAF za raundi ya kwanza dhidi ya Asas ya Djibouti ilipigwa jijini Dar es salaam sawa na mbili za Ligi Kuu.
Amesema mastaa wote wana ari ya kupata ushindi kutokana na mafuriko ya mashabiki wao ambao wanakwenda Rwanda kwa mabasi zaidi ya 15, kitu ambacho wanaamini ni kama deni kwao ili wasiwatie unyonge watakapokuwa wanarudi nyumbani kwa mchezo wa marudiano.
Amesema mashabiki hao wamewafanya kila mchezaji kujipanga kwa kuhakikisha wanakuwa na safari rahisi ya kurudi upitia furaha ya ushindi ambao wanataka kuutengeneza.
Tumeona video za mashabiki wetu wanaokwenda imetupa nguvu sana na kujiona kuna kitu kikubwa tunatakiwa kukifanya kuwapa furaha ya ushindi,” alisema Maxi aliyetua Jangwani msimu huu akitokea AS Maniema Union ya DR Congo ambaye ni kati ya wachezaji 26 waliosafiri jana Alhamis (Septemba 14).
Mchezaji pekee aliyekosekana kwenye safari hiyo ya Kigali ni nahodha, Bakar Mwamnyeto mwenye matatizo ya kifamilia, lakini mastaa waliosalia wameondoka sambamba na maofisa wa klabu hiyo wakiwamo makocha wanaoongozwa na Muargentina, Miguel Gamondi.