Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele amesema, ilikua lazima washinde katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Young Africans iliyocheza kwa kujiamini katika mchezo huo, iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 yakifungwa na Mshambuliaji Kennedy Musonda (Zambia) na Viungo Mudathir Yahya (Tanzania) pamoja na Tuisila Kisinda (DR Congo).
Mayele amesema walijiandaa vizuri kuelekea kwenye mchezo huo na waliamini watafanikiwa kutokana na kuamini walicheza na timu ya kawaida kama zilivyo timu nyingine, ambazo wamewahi kucheza nazo msimu huu.
Amesema hawana budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ushindi huo ambao umewapa alama tatu muhimu kwenye msimamo wa Kundi D, ambalo amekiri lina timu ngumu na zenye ushindani.
“TP Mazembe ni timu kama timu nyingine yoyote, tulijipanga kupata matokeo mazuri na tunamshukuru Mungu tumefanikiwa katika hilo, tumeshinda mabao matatu ambayo yana faida kubwa sana kwetu.”
“Sijali mimi kushindwa kufunga katika mchezo huu, kwanza timu inatakiwa kushinda ili kupata alama tatu, na hiyo inakuja kutokana na kucheza kitimu zaidi.”
“Mashabiki waendelee kutupa ushirikiano, tumefurahi sana kwa sababu walijitokeza kwa wingi Uwanjani kutushangilia katika mchezo wetu wa jana, ninaamini wameburudika na wamefurahi sana.” amesema Mayele
Kuhusu mchezo ujao, Meyele amesema anafahamu Young Africans inakabiliwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC na hana nafasi ya kuanza kuufikiria mchezo wa Kimataifa dhidi ya Real Bamako kwa sasa.
“Siufikirii mchezo wa kimataifa kwa sasa, ninajua mchezo unaofuata ni dhidi ya KMC FC, baada ya hapo nikiulizwa nitasema lingine lakini kwa sasa ninajua kuna mchezo Jumatano wa Ligi.”