Mshambuliaji mpya wa Young Africans Fiston Kalala Mayele, amewasihi Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kuacha kutoa lawama kwa wachezaji wao, kwa kisingizio cha ushindi wa bao moja.
Young Africans imekua ikipata ushindi wa bao moja tangu ilipoibamiza Simba SC kwenye mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii Septamba 25, hali ambayo imepokelewa tofauti na baadhi ya Wanachama na Mashabiki wenye uchu wa kuona kikosi chao kinapata ushindi mnono.
Mayele aliyesajiliwa Young Africans akitokea kwa Mabingwa wa DR Congo AS Vita Club amesema, Mashabiki na Wanachama hawapaswi kulaumu kwa nguvu zao zote katika kipindi hiki, kwa kisingizio cha ushindi wa bao moja kila wanapotinga dimbani.
Mashambuliaji huyo amesema bado kuna muda mrefu wa kufanikisha mpango wa kupata ushindi wa zaidi ya bao moja, hivyo Mashabiki na Wanachama wanapaswa kuwa wavumilivu, kwani mambo mazuri yanakuja.
Amesema jambo bora na la kujivunia kwao kwa sasa ni ushindi huo wa bao moja unaolalamikiwa, lakini wao kama Young Africans hawajaruhusu kufungwa hilo bao moja ambalo kwa Mashabiki na Wanachama ni kama shubiri.
“Ni mapema sana kulaumiwa, ukizingatia tunapata bao moja ni la ushindi hatujaruhusu kufungwa na katika bao hilo moja kunakuwa na nafasi nyingi zinazotengenezwa hivyo hii ni moja ya sifa kwetu kwamba tuna uwezo mkubwa tukitulia.” amesema Mayele.
Young Africans ilianza kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/22 kwa kuifunga Kagera Sugar bao 1-0, kicha ikashinda kwa idadi kama hiyo dhidi ya Geita Gold na mwishoni mwa juma lililopita waliifunga JKU ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki.