Mara baada ya kumalizika kwa pambano kati ya Tanzania dhidi ya Benin pale Uwanja wa Mkapa, mwandishi mmoja asiyejitambua alimfuata Mbwana Samatta na kumuuliza swali.

“Mashabiki wamekuwa wakisema wewe hauna mchango mkubwa ukirudi nyumbani tofauti na Ulaya.” Kudai kwamba mwandishi asiyejitambua ni kitu sahihi zaidi.

Huyu alikuwa mwandishi wa michezo au alikuwa mwandishi wa siasa? Huyu alikuwa mwandishi wa masuala ya jamii au alikuwa mwandishi wa masuala ya mazingira?

Hii ilikuwa ni mechi ya soka ambayo Mwandishi alikuwepo uwanjani. Mwandishi hana maoni yoyote ya maana licha ya kuutazama mpira kwa dakika tisini.

Wakati yeye ndiye ambaye alipaswa kutoa mwongozo kwa mashabiki, bahati mbaya yeye ndiye ambaye anapewa mwongozo na mashabiki.
Samatta anacheza vizuri akiwa na Stars ingawa kwa sasa hajafunga sana. Akiwa na Stars anacheza chini. Anachukua mipira, anakokota, anapiga pasi za kuunganisha timu.

Inawezekana anafanya haya kwa sababu ya timu yetu ilivyo. Alipokuwa kule Genk aliwahi kuniambia kwamba kocha wake alimtaka asimame katikati tu na kufunga.

Ni tofauti na mpira alioondoka nao akiwa Simba ambapo alikuwa anakokota kwa muda mrefu na kufunga. Kule walikuwepo kina Leon Bailey wa kumfanyia kazi hizi. Yeye alihitajika kusimama pale katikati tu.

Huku Tanzania Samatta anacheza ule mpira wake wa zamani. Kuna akina nani zaidi wa kumfanyia kazi? inabidi pia ajifanyie kazi nyingi ambazo Ulaya huwa anafanyiwa zaidi na kujikuta akiwa mviziaji.

Mwandishi hawezi kuliona hili kwa sababu kila mtu anasubiri Samatta afunge tu basi. Samatta asipofunga anabebeshwa mzigo wa lawama mitaani na katika mitandao ya kijamii.

Ni kitu cha kawaida kwa sababu amekuwa mhanga wa ukubwa wake. Na hasa linapokua suala kwamba yeye ni Mtanzania. Watanzania wamezoea lawama. Hawawapendi watu wao ambao wamekuwa wakubwa.

Samatta anastahili heshima kubwa nchi hii. ameamsha ndoto za vijana wengi ambao waliona kuna baadhi ya mambo hayawezekani.

Imeandaliwa na Edo kumwembe

Van Gaal amsikitikia Koemen, De Jong
Mayele awatuliza mashabiki Young Africans