Wachezaji wa Klabu za Simba SC na Young Africans Fiston Mayele, Kenedy Musonda, Clatous Chama na Henock Inonga wameondoka Dar es salaam leo Jumatatu (Machi 20) kwa ajili ya kuitikia wito wa Makocha wa Timu za Mataifa ya DR Congo na Zambia.
Wachezaji hao wametajwa katika vikosi cha timu za mataifa hayo kwa ajili ya Michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ itakayocheza mwishoni mwa juma hili na juma lijalo.
Wachezaji hao wamekwenda katika mataifa yao kupitia Nairobi, Kenya, ambapo wakiwa mjini hapo watapanda Ndege tofauti kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani.
Wakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, wachezaji hao walipiga picha ya pamoja ambayo imeshambazwa katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo Kiungo Clatous Chama ametoa ufafanuzi wa picha hiyo kwa kusema Mpira huwa ni ushindani kwa mda ule wanapokuwa Uwanjani tu (dakika 90) ila baada ya hapo wao ni marafiki na maisha ya kawaida yanaendelea.
Fiston Mayele na Henock Inonga wameitwa katika kikosi cha DR Congo ambacho kinatarajia kucheza mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi I dhidi ya Mauritania itakayokuwa ugenini Japoma Stadium, mjini Douala (Cameroon) Machi 24.
Mchezo wa Mzunguuko wanne utazikutanisha tena timu hizo Machi 29, katika Uwanja wa Cheikha Ould Boïdiya, mjini Nouakchott.
Kwa upande wa Kenedy Musonda na Clatous Chama wameitwa kwenye kikosi cha Zambia ambacho kina kazi ya kuikabili timu ya taifa ya Lesotho katika Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola.
Timu hizo zitakutana tena katika mchezo wa Kundi H Machi 26 katika Uwanja wa Dobsonville mjini Johannesburg (Afrika Kusini).