Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), limetangaza kuendesha mafunzo kwa makocha yakiwa na lengo la kuongeza idadi ya walimu wa mchezo huo. Makocha hao wataongezwa kupelekwa kuwanoa wanamasumbwi ambao watashiriki katika michuano mbalimbali ya kimataifa.

Rais wa BFT, Lukelo Wililo, amesema shirikisho linataka kuongeza idadi ya makocha wenye utaalamu wa ndondi ambao watatoa mafunzo yatakayoimarisha uwezo wa mabondia.

Wililo amesema mafunzo hayo yataendeshwa na wakufunzi kutoka taasisi ya ‘Refocus Africa’ ambayo iliingia mkataba wa mwaka mmoja na BFT kuwafundisha makocha wa masumbwi.

Amesema wakufunzi hao watakuja nchini kuendesha kozi za makocha kulingana na makubaliano ya kimkataba.

“BFT inaamini kuwa kupatikana kwa idadi kubwa ya makocha kuanzia ngazi za awali kunaweza kusaidia kuimarisha mchezo wa ngumi za ridhaa nchini,” amesema Wililo.

Rais huyo amesema maandalizi ya mafunzo yanaendelea na yakikamilika, kozi itaendeshwa jijini Dar es Salaam.

Simbu: Bado nina deni kubwa kimataifa
Taifa Stars yawasili salama Misri