Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele amesema Kiungo wa Simba SC Mzamiru Yassin alimpigia simu na kumuomba radhi kufuatia Rafu aliyomchezea wakati timu zao zilipokutana Jumapili (April 16) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mayele amefichua siri hiyo dakika chache kabla ya kikosi cha Young Africans kuanza safari ya kuelekea Nigeria mapema leo alfajiri jijini Dar es salaam.
Mshambuliaji huyo amesema kwa sasa anaendelea vizuri na ana matarajio ya kuwa sehemu ya kikosi kitakachopambana na Rivers United katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Jumapili (April 23).
“Nilipata injury kidogo, nadhani nilipata na muda wa kupumzika na nilianza mazoezi leo kwa sababu nilipata maumivu sana upande wa kiuno.”
“Mtu aliyefanya hivyo (Mzamiru) alinipigia simu nikaongea nae, kaniambia hajafanya makusudi ni bahati mbaya imetokea, kwenye football inatokea. Nimeanza mazoezi mepesi na nitakuwa sehemu ya timu Inshallah” amesema Mayele
Young Africans ilitinga hatua ya Robo Fainali baada ya kuongoza msimamo wa Kundi D kwa kufikisha alama 13, sawa na US Monastir ya Tunisia iliyomaliza nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.