Aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, Senzo Mazingisa Mbatha amekabidhi ofisi na nyaraka za klabu hiyo.
Kabla ya kukabidhi nyaraka za waajiri wake wa zamani, Juzi Jumatatu Mshauri Mkuu wa Mwenyekiti wa Bodi, Crescetius Magori alisema Senzo tangu atangaze kujiuzulu alikuwa hapatikani hewani kwa maana ya kwamba simu zake za mkononi zilizimwa.
Hivyo kupitia taarifa hiyo, Magori alimtaka Senzo kwenda kukabidhi ofisi kama utaratibu wa kazi ulivyo sehemu yoyote ambayo mtu anaajiriwa.
Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, amethibitisha kuwa Jana Jumanne Agosti 11, 2020, Mazingiza alitinga ofisini hapo na ilipofika mishale ya jioni aliabidhi kila kitu.
“Amekabidhi ofisi kama utaratibu ulivyo wa kazi, ni kweli hakupatikana hewani na alikuja tu kwa kushitukiza, kikubwa ni hilo kukabidhi ili maisha mengine yaendelee,” amesema mjumbe huyo.
Kuhusu mbadala wake, kigogo huyo amesema; “Kuna kikao kinaendelea leo Jumatano ambacho wanajadili nani atakaimu kwa wakati huu huku mchakato mwingine wa kutangaza ajira ukifuata hapo baadaye.
“Nafasi ya CEO ni ya kuajiriwa hivyo taratibu zote za ajira zinapaswa kufuatwa, ni lazima kutuliza akili kufanya hivyo, lakini mtu wa kukaimu atapatika na huenda akatangazwa hata leo hii hii,”
Imeelezwa kwamba mtu atakayepatikana kukaimu nafasi hiyo kutoka ndani ya kikao hicho hapaswi kutoka kwenye Bodi ya Wakurugenzi, yaani asiwe mjumbe wa bodi hiyo ambapo Magori ni miongoni mwa wanaotajwa kukaimu kiti hicho.