Rais mteule wa Kenya, William Ruto amesema amefanya mazungumzo na rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta, na zaidi imekuwa ni maongezi kuhusu uchaguzi wa Agosti 9 na makabidhiano ya madaraka.

Katika mtandao wake wa Twitter, Ruto ameandika, “Nimekuwa na mazungumzo ya simu na bosi wangu, Rais Uhuru Kenyatta. Tumezungumza juu ya uchaguzi uliopita na namna ya kukabidhiana madaraka kama ambavyo taratibu na tamaduni zetu zinataka,”

Jumatatu Agosti 5 baada ya Mahakama kuhalalisha ushindi wa Ruto, alisema hajazungumza na Kenyatta kwa miezi kadhaa Ingawa aliahidi kumpigia simu.

Rais Uhuru Kenyatta akiongea na simu. Picha na Ikulu ya Kenya

Ruto katika hotuba zake baada ya kutangazwa ushindi wa Urais, alisema kuwa anaendelea kuheshimu na kuthamini muunganiko wake na Uhuru ingawa hakumuunga mkono katika uchaguzi na kumpigia kura.

“Nilipomchagua Uhuru Kenyatta, sikumchagua kwa sababu yoyote, hivyo sikwazwi na yeye alipoamua kumchagua na kumshika mkono mtu mwingine katika Uchaguzi huu hivyo tutabakia marafiki katika mazingira tuliyonayo,” alisema Ruto.

Ofisi ya Rais nchini Kenya imetangaza kuwa ipo katika maandalizi ya makabidhiano ya madaraka na shughuli hiyo imepangwa kufanyika Septemba 13 ambayo imetajwa kama siku ya mapumziko ili wakenya washuhudie uapisho huo wa Ruto.

TEF: Mchakato mabadiliko Sheria ya Habari ni wa wote
Bunge latangaza kuongeza muda hali ya hatari