Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Habari si wa TEF pekee, bali ni muunganiko wa taasisi mbalimbali vikiwemo vyuo vya uandishi na idara za Habari.

Meena ameyabainisha hayo, wakati akizungumza na wakuu wa idara kutoka vyuo Vikuu na vyuo vya Uandishi wa Habari, kuhusu hatua zilizofikiwa juu ya mchakato wa mabadiliko ya sheria ya Habari nchini.

Amesema, “Sula hili ni letu sote si la TEF pekee, na baada ya sheria hii kusainiwa na kuanza kutumika, wadau wa habari tulianza kuipinga ingawa awali hatukupata ushirikiano kama ilivyo sasa.’’

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena akifafanua jambo katika mkutano na wakuu wa idara kutoka vyuo Vikuu na vyuo vya Uandishi wa Habari, kuhusu hatua zilizofikiwa juu ya mchakato wa mabadiliko ya sheria ya Habari nchini.

Meena ameongeza kuwa, muundo wa vyombo vilivyoelekezwa na sheria iliyopo unaweza kuvunjwa na kuunda chombo kimoja, ambacho kitakuwa imara na kusimamiwa kisheria kama ilivyo katika taaluma nyingine.

Aidha, kupitia mazungumzo hayo, mjumbe huyo wa TEF aliwaonesha washiriki baadhi ya vipengele vilivyomo kwenye nakala ya mapendekezo ya mabadiliko hayo, na kutaka kuondolewa kwa uwingi wa vyombo vinavyosimamia tasnia ya habari.

“Sheria inataja kuwepo kwa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Vyombo vya Habari na mfuko wa waandishi sasa kuwa na vyombo vyote hivi vinavyofanya kazi ya aina moja, tunasema hapana,” amefafanua Meena.

Baadhi ya Washiriki wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, (hayupo pichani) aliyekuwa akizungumzia mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Habari.

Hata hivyo amesema, ‘‘Hapa tunashauri tuwe na chombo kimoja ambacho kitafanya kazi zote hizo kama ilivyo kwa taaluma za uanasheria, uhasibu, ukandarasi na nyingine ambao hawana utitiri wa vyombo.’’

Awali, akizungumzia ukomo wa adhabu ulioweka na sheria hiyo, Meena alisema sheria ya habari ya mwaka 2016 inaweka adhabu isiyopungua miaka mitatu jela na kwamba, haimpi nafasi hakimu kutoa adhabu chini ya miaka hiyo hata kama kosa ni dogo.

Kocha Zoran Maki aacha ujumbe Simba SC
Kenya: Mazungumzo ya simu Ruto na Kenyatta yafichuka