Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain Kylian Mbappe amefanikiwa kuvunja rekodi iliyokua inashikiliwa na Lionel Messi, na kuwa mchezaji mwenye umri mdogo aliyefiksha mabao 15, kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 20, alifunga mabao matatu kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya usiku wa kuamkia leo, ambapo PSG walichomoza na ushindi wa mabao matano dhidi ya Club Brugge iliyokua nyumbani.
Mabao mengine ya PSG kwenye mchezo huo yalifungwa na washambuliaji kutoka Argentina Mauro Icardi na Angel Di Maria.
Mbappe ameweka rekodi ya kupachika mabao 15 kwenye ligi ya mabingwa barani Ulaya, akiwa na umri wa miaka 20 na siku 306, akimpuku Messi ambeya alifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 21 na siku 288.
Kabla ya Messi kushikilia rekodi hiyo, mshambuliaji nguli wa Real Madrid Raul Gonzalez alifikia mafanikio hayo akiwa na umri wa miaka 22 na siku 163.
Mbappe pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao matatu akitokea benchi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, akichukua sifa hiyo kutoka kwa Joseba Llorente wa Villarreal, ambapo alifanya hivyo Oktoba 2008 dhidi ya Aalborg.