Leo Septemba 21, 2018 Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR Mageuzi, James Mbatia amezungumza na vyombo vya habari na kuilalamikia Serikali kuwa imeshindwa kulinda na kuokoa watanzania wakati majanga yanapotokea.
Na kusema kuwa Tanzania imepata janga kubwa sana ambalo haliwezi kuzibwa kwa namna yeyote.
”Hasara iliyotokana kwa kuzama kwa MV Nyerere huwezi kuilinganisha na kitu chochote hata tukiuza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huwezi kurudisha uhai wa wananchi waliopoteza maisha” amesema Mbatia.
Serikali ilitakiwa kumsikiliza muwakilisha wa ukerewe na ijitafakari kwani alivyoleta hoja hiyo bungeni Serikali haikumpa majawabu sahihi namna ya kupambana, kuwalinda na kuwaokoa wananchi ndiyo maana majanga yametokea, ameongezea Mbatia.
Pia amelaumu uongozi mzima ulioruhusu ukiukwaji wa sheria wakati wa utumiaji wa kivuko cha MV Nyerere ikiwa ni pamoja na kuruhusu kivuko hiko kubeba idadi kubwa ya abiria na mizigo kulinganisha na uwezo wake.
Mbatia amesema kwamba ifike mahali Tanzania iache kuishi kwa matukio ambayo yanakuja na kuondoka kisha yanasahaulika.
Aidha, Mbatia amesema amewahi kushauri Serikali kutenga fedha katika bajeti ya mwaka huu ili kuanzisha mawakala wa kujitegemea watakaojihusha na masuala ya uokoaji pindi majanga yatakapotokea wakati wowote kwa lengo la kuwaokoa watanzania.
Na ametoa pole kwa wana Ukerewe na amewaomba wahusika katika zoezi la uokoaji linaloendelea kufanya kazi yao vyema na kwa weledi.