Wakati Mashabiki wa Soka nchini Tanzania wakisubiri Kandanda la Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Singida Big Stars, Mchezo huo umeteka hisia za upinzani kwa pande zote mbili.
Young Africans iliyoshushwa kileleni jana Jumanne (Novemba 15) na Azam FC iliyochomoza na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, itahitaji kushinda kesho Jumatano (Novemba 17) ili kuendeleza Rekodi ya UNBEATEN na kurejea kileleni, huku Singida Big Stars ikihitaji ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuwania nafasi nne za juu katika msimamo.
Mbazil wa Singida Big Stars Bruno Gomez amesema wapo tayari kuikabili Young Africans kwenye mchezo wa kesho Jumanne (Novemba 16) utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa mishale ya saa moja usiku.
Kiungo huyo amesema wamejiandaa vya kutosha na wanaamini wataipa upinzani wa kweli Young Africans, na ikiwezekana kuvunja UNBEATEN yao iliodumu kwa zaidi ya msimu mmoja.
“Ni ngumu kucheza na Young Africans ambaye ndio Bingwa Mtetezi, ingawa haitufanyi kuingia kwa kuwahofia, tunawaheshimu sana kwa sababu ya wachezaji wazuri walionao, japo hata sisi ni bora kama walivyo wao pia.”
“Mchezo wetu uliopita dhidi ya Simba SC ulitupa mwanga na jinsi ya kukabiliana na Presha pindi tunapocheza na aina ya timu kubwa, hivyo kwetu ilikuwa ni somo japokuwa tulicheza uwanja wa nyumbani tofauti na Young Africans ambapo tutakua ugenini.” amesema Bruno
Kwenye Michezo 10 iliyocheza Singida Big Stars imeshinda mitano, sare tatu na kufungwa miwili ikiwa nafasi ya nne ikifikisha alama 18, huku Young Africans iliyocheza michezo tisa imeshinda saba na sare mbili ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.