Katika kuhakikisha linakomesha matukio ya ajali kuelekea mwishoni mwa mwaka, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeendelea kutoa Elimu kwa madereva na kuwafungia leseni madereva watano kwa makosa mbalimbali ikiwemo ulevi na mwendokasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP. Justine Masejo ameyasema hayo hii leo Novemba 16, 2022 na kusema madereva hao wamefungiwa leseni zao kwa muda wa miezi mitatu hadi sita kwa makosa ya ulevi, mwendokasi, kusababisha ajali, wenye makosa yanayojirudia na wanaoyapita magari mengine sehemu hatarishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP. Justine Masejo.

Kuhusu utoaji wa Elimu, Kamanda Masejo amesema, Jeshi hilo limefanikiwa kutoa elimu katika nyumba za ibada, stendi za mabasi, mashuleni, vijiwe vya bodaboda pamoja na masoko ambapo jamii hiyo imepata uelewa wa kuhusiana na sheria mbalimbali za usalama barabarani.

Hata hivyo, Masejo ametoa onyo kwa madereva wanaoendelea kuvunja sheria za usalama barabarani kwamba Polisi haitamvumilia dereva yeyote kwa makosa ya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani na kuwaomba wananchi kutoa taarifa za uhalifu na walifu.

Kocha Singida Big Stars atamba Dar es salaam
Mbazil Singida Big Stars atuma ujumbe Young Africans