Manchester City ya England na Real Madrid ya nchini Hispania, leo Jumatano (Mei 17) zitashuka dimbani kuonyeshana ubabe katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, msimu huu 2022/23.
Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Etihad jijini Manchester, England saa 4:00 kwa saa za Afrika Mashariki.
Kipute hicho cha aina yake kinatarajiwa kuamuliwa na mwamuzi Szymon Marciniak kutoka Poland, mwenye umri wa miaka 42.
Timu hizo zitashuka dimbani zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa juma lililopita katika Uwanja wa Santiago Bernabeu, mjini Madrid nchini Hispania.
Katika mchezo huo, bao la Real Madrid lilifungwa na Mbrazili Vinicius Jr huku Mbelgiji Kevin De Bruyne akiisawazishia Man City.
Mshindi wa mchezo wa leo atatinga Fainali na kuvaana na Inter Milan iliyoibuka na ushindi wa jumla wa 3-0 dhidi ya AC Milan
Timu hizo kutoka Italia zilivaana jana saa 4:00 usiku katika Uwanja wa Giuseppe Meazza jijini Milan huku Inter ikiibuka na ushindi wa 1-0 ambao ni muendelezo wa ushindi wa mchezo wa mkondo wa kwanza wa mabao 2-0.