Kamati ya kuchunguza tuhuma zinazoelekezwa kwa mlinda mlango wa Mbao FC Erick Ngwengwe, inatarajiwa kukabidhi ripoti kwa uongozi wa klabu hiyo mwishoni mwa juma hili.
Kamati ya kumchunguza mlinda mlango huyo, iliundwa na uongozi wa Mbao FC siku moja baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba kwa kufungwa mabao matatu kwa mawili kwenye uwanja wa CCM Kirumba mwanzoni mwa juma lililopita.
Afisa habari wa Mbao FC Crinstant Malinzi amezungumza na Dar24, ambapo amesema kamati hiyo inafanya kazi yake bila kuingiliwa na mtu yoyote, kutokana na hitaji la kutaka kufahamu ukweli wa tuhuma zilizoelekezwa kwa Erick mara baada ya mchezo dhidi ya Simba.
“Kamati inafanya kazi yake kwa uweledi na haiingiliwi na mtu yoyote, kwa sababu tunataka kujiridhisha kama kweli mlinda mlango wetu alihusika kufungisha kwa makusudi katika mchezo ule.”
“Wajumbe wa kamati wanatoka ndani ya klabu yetu na hatukutaka kumshirikisha mtu mwingine yoyote, lakini kama itahitajika kumuongeza mtu mwingine kutoka hapa Mwanza tutafanya hivyo.” Amesema Malinzi.
Mlinda mlango Ngwengwe alisimamishwa kwa muda usiojulikana ili kupisha uchunguzi unaofanywa dhidi yake.
Katika mchezo dhidi ya Simba, Mbao FC walikua wakiongoza mabao mawili kwa sifuri hadi katika dakika ya 82, lakini walishindwa kuhimili mashambulizi yaliyofanywa langoni mwao dakika zilizosalia na kujikuta wakifungwa mabao matatu.