Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amezungumzia maendeleo ya afya ya mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu aliyelazwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi baada ya kupigwa risasi.
Akizungumza jana jioni kutoka jijini Nairobi, Mbowe amesema kuwa afya ya Lissu imeendelea kuimarika taratibu.
“Ni kweli mgonjwa alizungumza jana kwa mara ya kwanza tangu ametoka Dodoma. Leo hali yake inaendelea kuimarika lakini inaimarika kwa taratibu sana kwa sababu kwakweli ana majeraha makubwa sana,” Mbowe aliiambia Azam TV.
Ameongeza kuwa ingawa gharama za matibabu ni kubwa lakini wanajaribu kwa kadiri iwezekanavyo kwa kuwashirikisha wananchi ndani na nje ya nchi kuweza kuokoa maisha ya Lissu kwani wanaamini mchango wake katika Taifa ni mkubwa kuliko fedha zitakazotumika.
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema kuwa dereva aliyekuwa na Lissu wakati wa tukio la kupigwa risasi ambaye jeshi la polisi lilitangaza hivi karibuni kuwa linamtafuta, amelazwa pia jijini Nairobi.
“Unajua dereva huyo alikuwa na mheshimiwa Lissu wakati tukio linatokea. Kwahiyo katika mazingira haya amekuwa na msongo wa mawazo na vilevile hofu ya usalama wake kwakuwa hatujui hao wauaji watakuwa na nia gani kuhusu yeye,” alisema Mbowe.
Amesema kuwa dereva huyo ambaye majina yake halisi ni Simon Mohamed Bakari atarejea nchini baada ya kupatiwa matibabu na ushauri nasaha kuhusu hali yake ya msongo wa mawazo.
Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 wiki iliyopita akiwa ndani ya gari lake, muda mfupi baada ya kuwasili nyumbani kwake eneo la Area D mjini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jeshi la polisi limesema limeongeza nguvu ya wapelelezi mjini humo kuwasaka waliohusika katika tukio hilo.