Waandaaji wa tamasha la Fiesta na wadhamini wakuu wa tamasha hilo ambao ni kampuni ya simu za mkononi ya Tigo wamekanusha taarifa zilizotolewa na Mwana FA kuwa alizuiwa kuingia kwenye tamasha hilo jijini Arusha.

Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba amesema kuwa hakuna mtu yeyote anayezuiwa kuingia kwenye tamasha hilo kwani wao ni wafanyabiashara.

Naye Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael ameungana na kauli ya Ruge akieleza kuwa kila mwenye tiketi anaruhusiwa kuingia kwenye tamasha hilo.

“Hakuna anayezuiwa kuingia kwenye tamasha. Hatukumzuia mtu yeyote mwenye tiketi kuingia tamashani,” Shisael anakaririwa na Mwananchi.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa FA aliingia ndani ya tamasha hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Arusha lakini alizuiwa kukaa katika eneo la watu maalum (VIP) kwani hakuwa na kibali au tiketi maalum ya kuwa katika eneo hilo.

Awali, Mwana FA aka Choir Master alitumia mtandao wa Twitter kueleza kuwa alizuiwa kuingia kwenye tamasha hilo, akihusisha hatua hiyo na hatua za kushinda kesi ya kutakiwa kulipwa zaidi ya shilingi bilioni 2 na kampuni ya Tigo kwa kutumia nyimbo zao kama miito ya simu bila ridhaa yake na swahiba wake, AY.


Naye AY alikumbusha kuwa mwaka jana kampuni ya Tigo ilipiga marufuku nyimbo zao kutochezwa katika tamasha hilo wakati wasanii wengine wakijiandaa kutumbuiza.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Septemba 11, 2017
Mbowe aeleza mapya ya hali ya Lissu, Dereva wake naye alazwa