Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amezungumza kwa mara ya kwanza kwa undani kuhusu kile anachodai ni sababu ya aliyekuwa Mgombea urais wa chama hicho mwaka 2015, Edward Lowassa kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza kwenye mkutano wa ndani wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni Singida Kaskazini, Mbowe alisema kuwa Lowassa alihama baada ya kushindwa kuhimili mikiki-mikiki ya upinzani.
Mbowe alisema kuwa Lowassa alishindwa kutoa matamko kadhaa kama mgombea urais wa chama hicho hata baada ya kukatazwa kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wapiga kura milioni sita waliomuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu.
Alikumbushia kuwa mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Waziri Mkuu alikaa kimya baada ya kupata misukosuko iliyotokana na kauli aliyoitoa mwaka 2017 akitaka masheikh wanaoshikiliwa gerezani kuachiwa huru au kushtakiwa kama wana makosa, kauli iliyomsababisha kuhojiwa polisi.
Mbowe anadai kuwa Lowassa alimpigia simu akionesha kushangazwa na hatua hiyo na kwamba baada ya kuhojiwa hakuwahi kuzungumza tena hadi alipokihama chama hicho.
“Ilifika mahali mzee akaona huku ni balaa, misukosuko, mali zikapotea,” alisema Mbowe.
“Lakini Lowassa alipokuja Chadema alikuja na watu, lakini alivyoondoka aliondoka yeye na mkewe na watoto wake wawili kwa sababu tumejenga chama taasisi,” aliongeza.
Machi 1 mwaka huu, Lowassa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alitangaza kurejea CCM. Hakutoa sababu nyingi zaidi ya kurejea ny umbani.
“Msiniwekee maneno mdomoni. Nawashukuru wote walioniunga mkono, nawashukuru wanachama wote wa Chadema. Mimi nimerudi nyumbani,” alisema Lowassa alipofika Monduli ambako ni nyumbani kwake.