Matokeo ya uchaguzi Chadema yameeleza kuwa Freeman Mbowe ameshinda nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho Taifa, kwa kuibuka na kura 886 sawa na asilimia 93.5 ya kura dhidi ya Cecil Mwambe aliyepata kura 59 sawa na asilimia 6.2 huku kura 3 zikiharibika.
Mwenyekiti huyo ataongoza Chadema kwa miaka mingine mitano, itakumbukwa kuwa yupo kwenye usukani wa chama hicho kwa miaka 15 sasa huku mara kadhaa amekuwa akishinda kwa kishindo na kwa mara ya mwisho 2014 alishinda kwa asilimia 97.3 dhidi ya Gambaranyera Mangateo.
Aidha, kwenye uchaguzi wa jana, Tundu Lissu amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti Taifa (bara), ambapo licha ya Sophia Mwakagenda kujitoa mwishoni, amepata kura 11 sawa na asilimia 1.2 huku Lissu akipata kura 930 sawa na asilimia 98.8 na kura zilizoharibika ni 9.
Kwa upande wa Zanzibar, Said Mohamed ameshinda nafasi ya makamu mwenyekiti Taifa, iliyokuwa na mgombea mmoja, kwa kura za ndio 839 sawa na asilimia 88.7 huku kura za hapana zikiwa 95 sawa na asilimia 10 na zilizoharibika ni 12.