Mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa hajaridhishwa na namna inavyoendeshwa kesi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu CHADEMA kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga iliyoahirishwa.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, ambapo amezitaka mamlaka husika zinazosimamia sheria kujiangalia upya kuhusu utendaji kazi wake.
“Tumesikitishwa kwa namna suala hili jinsi lilivyo shughulikiwa, sipendi kuingilia uhuru wa Mahakama, mienendo ya kimahakama lakini mimi kama raia na kiongozi nafikiri vyombo vinavyostahili kutoa haki kwa wananchi vinawajibu wa kujiangalia vizuri. Mahakimu, Majaji, Mawakili wa Serikali pamoja na Askari wenyewe hawa wote ni binadamu haina maana kwamba wao hawawezi kufanya makosa wao ni binadamu kama walivyo wengine,”amesema Mbowe
Hata hivyo, Kesi inayowakabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu CHADEMA kanda ya Nyasa Emmanuel Masonga imehairishwa na kutajwa kusikilizwa Februari mbili baada ya Mawakili watatu kujitoa kuwasimamia katika kesi hiyo.