Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko , amesisitiza tena kuhusu hoja yake ya Novemba mwaka jana bungeni, kwamba kutokana na kushamiri kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto,anafikiria kuwa wanaobainika kufanya hivyo wahasiwe ili kuifanya jamii ya kitanzania kuwa salama.
Akichangia mjadala huo bungeni April 12, 2022 mbunge huyo amesema kuna haja serikali kufanya marekebisho ya sheria ili kuwe na adhabu kali zaidi dhidi ya wanaonajisi watoto, mojawapo ni kuhakikisha wanaopatikana na hatia wanahasiwa ili kuwa fundisho kwa wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.
Jumatano ya wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, aliliambia Bunge matukio 27,838 ya vitendo vya ukatili nchini yameripotiwa kwenye vituo vya polisi nchini katika miaka minne iliyopita.
Katika matukio hayo vitendo vya ubakaji vimekithiri kwa kuwa na matukio 19,726, huku akifafanua kuwa kuanzia mwaka 2019 hadi Machi, 2022, kulikuwa na matuko ya ubakaji 19,726, kulawiti 3,260 yaliyotendwa dhidi ya wanaume 3,077 na wanawake 183.