Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umewaelekeza mabalozi kufanya kazi kwa bidii na weledi pamoja na kuweka maslahi ya Taifa mbele katika utekelezaji wa majukumu yao.

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara Balozi Joseph Sokoine wakati walipokutana na mabalozi wanne walioapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan tarehe 10, 2022.

Akiwaasa Mabalozi hao, Waziri Mulamula alisisitiza kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ni kiungo muhimu kati ya Serikali na dunia hivyo mawasiliano ya ndani na nje ya Wizara yafanyike kwa weledi na wakati kwa kuzingatia viwango vya taifa na kimataifa.

Waziri Mulamula aliongeza kuwa matarajio ya Rais kwa kuwaapisha Mabalozi vijana ni kwamba wataimarisha utendaji kazi wa Wizara kuendana na kasi yake, hivyo ni muhimu kuchapa kazi bila urasimu.

“Pale ambapo mnaweza kuweka ubunifu, fanyeni hivyo, leteni mawazo mapya milango yetu ipo wazi wakati wote ili tupige hatua”

Naye Katibu Mkuu wa Wizara aliongeza kuwa Mabalozi hao watapangiwa majukumu mengine ya kutoa mihadhara kwenye Chuo cha Diplomasia kwa watumishi wapya lakini pia Mabalozi hao wawe kiungo baina ya Taasisi zilizo chini ya Wizara na Taasisi nyingine Serikalini kama vile Chuo cha Diplomasia (CFR) na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC)

Kwa mujibu wa viongozi hao, vyeo vya mabalozi hao ni: Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa (Director of Multilateral Cooperation), Balozi Macocha Tembele, Mkurugezi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Director of Government Communication) Balozi Mindi Kasiga, Mkurugenzi Kazi Maalum (Ambassador Special Duties), Balozi James Bwana pamoja na Mkufunzi Mwelekezi Mwandamizi (Senior Directing Staff – Foreign) wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Balozi Noel Kaganda.

Hassan Dalali: Tupeni nafasi tuzungumze na wachezaji
Mbunge asisitiza wanaonajisi watoto wahasiwe