Mahakama ya kijeshi katika Nchi ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, imemhukumu adhabu ya kifo Mfanyabiashara wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Kitaifa wa eneo la Masisi, Edouard Mwangachuchu (70), kwa kosa la uhaini.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji mfawidhi Jenerali Robert Kalala amesema Mwangachuchu (ambaye hakuwepo wakati ikisomwa hukumu hiyo), alipatikana na hatia ya uhaini kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria na kushiriki katika harakati za uasi wa kundi la M23.
Hata hivyo, uamuzi huo umekosolewa vikali na wakili wake aliyesema umechochewa na chuki ya kikabila huku Mahakama hiyo ikiamuru kuachiwa mara moja kwa mshtakiwa mwenza ambaye ni Afisa wa Jeshi la Polisi Nchini humo, Robert Muchamalirwa.
Adhabu ya kifo katika Nchi ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, mara nyingi hutolewa lakini haijatumika kwa miaka takriban miaka 20 sasa na badala yake Mjaji hutoa hukumu au adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mtu anayepatikana na hatia ya makosa ya namna hiyo.