Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata nafuu katika huduma za afya, Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad amekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 12.6 katika vituo vya afya vinne.

Vituo vilivyo nufaika na msaada huo ni pamoja na Nhobola, Songwa, Ng’wang’haranga na Dulisi vilivyopo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga

Aidha, amevitaja vifaa tiba hivyo kuwa ni viitanda sita vya kisasa vya kujifungulia kwa akina mama wajawazito,vitanda sita kwa ajili ya kulalia wagonjwa, shuka 12 na viti sita kwa ajili ya wagonjwa.

Azza amesema kuwa vifaa hivyo vimetolewa na ubalozi wa China nchini Tanzania na vitasaidia katika kupunguza adha wanayopata akina mama wajawazito wanapofika kupata huduma katika vituo vya afya.

“Akina mama ndiyo wanaopata adha kubwa wanapohitaji huduma za afya, baada ya kuona jinsi akina mama hawa wanavyoteseka, niliamua kuanza kutafuta watu wa kutusaidia, nashukuru ubalozi wa China nchini ulikubali kunipatia vifaa hivi kwa ajili ya wananchi wa Shinyanga”,amesema Azza.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi kuachana na tabia ya kuozesha watoto wadogo kwa tamaa ya mali, ng’ombe’ kwani takwimu zinaonesha kuwa watoto wanapopata ujauzito inasababisha wengi wao kupoteza maisha wakati wa kujifungua.

 

Dkt. Nchimbi atoa agizo kwa mkurugenzi wilaya ya Singida mjini
Wadau wa madini watakiwa kujikita katika uzalishaji