Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting Mbwana Makata alisema hawajakata tamaa na wanaendelea na maandalizi ya michezo iliyosalia kabla ya msimu huu 2022/23 haujafikia tamati.
Ruvu Shooting inaburuza mkia wa Ligi Kuu Tanzania bara ikiwa na alama 20, ikicheza michezo 27 hadi sasa.
Kocha Makata amesema : “Tutaendelea kujiweka sawa kwa michezo iliyobaki, niaamini wachezaji wangu watapambana hadi mwisho, tulipo sasa sio pazuri lakini hatujakata tamaa.”
Mara ya mwisho Ruvu Shooting ilishuka 2014/15 pamoja Polisi Tanzania iliyokuwa ikiburuza mkia kwa alama 25 huku Toto African na African Sports zikipanda Ligi Kuu.
Ruvu Shooting ilirejea Ligi Kuu 20l6/17 sambamba na Mbao FC na kumaliza msimu ikiwa nafasi ya saba na alama 36 huku Mbao ikimaliza ya 12 kwa alama 33.
Msimu huo Young Africans ilibeba ubingwa kwa kuvuna alama 68 sawa na Simba SC iliyomaliza ya pili lakini uwiano wa mabao ndio uliwabeba Wananchi waliokuwa na wasatani wa mabao 43 dhidi ya 33 ya Mnyama.
Hadi sasa zimesalia mechi tatu dhidi ya Simba. Singida Big Stars na kufunga msimu Mei 28 dhidi ya Dodoma Jiji itakayokuwa nyumbani.
Ruvu Shooting ndio timu yenye safu mbovu zaidi ya ushambuliaji kwani katika michezo 27 imefunga mabao 18 na kufungwa 36 baada ya kushinda michezo mitano sawa na sare.
Kinara wa mabao kikosini ni Abalkassim Suleman mwenye mabao manne, huku Valentino Mashaka na Abralham Mussa kila mmoja akiwa na mawili, Ally Bilaly, Rolland Msonjo, William Patrick, Samson Joseph, Mgandila Shaban na Michael Aidan kila mmoja bao moja.