Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Ally Samatta anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti juma lililopita huko nchini Ubelgiji.
Samatta alilazimika kukosa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Benin uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja, kufuatia majeraha ya goti ambayo yalipelekea kufanyiwa upasuaji ambao ulifanikiwa kwa asilimia 100.
Kwa sasa mshambuliaji huyo ameanza kufanya mazoezi mepesi, baada ya kutembelea magongo kwa siku kadhaa, na hali hiyo imetafsiriwa huenda ikamuwezesha kurejea uwanjani tofautu na muda aliokua amepangiwa na jopo la madaktari wa klabu KRC Genk.
Samatta amethibitisha hilo kupitia mitandao ya kijamii kwa kueleza anaendelea vizuri, na anatarajia kuendelea kufanya mazoezi mepesi kwa siku kadhaa kabla ya kupangiwa utaratibu mwingine ambao utamwezesha kurejea kwenye hali yake ya kawaida.
“Naanza kuhisi nafuu mapema sana, leo nimejaribu kuziacha nyuma kwa sekunde kadhaa fimbo na kutembea,”amesema Samatta aliyefanyiwa upasuaji wa goti hilo Novemba 10 mjini Genk, Ubelgiji.
Samatta anaelekea kumaliza juma la kwanza kati ya majuma sita ya mapumziko kufuatia kuumia Novemba 4, mwaka huu alipokua akiitumikia klabu yake, KRC Genk ambayo ililazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
Baada ya kufanyiwa vipimo ikagundulika Samatta ameumia kwenye mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia ambayo ilichanika, hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji mdogo ili apone sawia.
Samatta aliumia akichezea mchezo wa 70 akiwa na KRC Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).