Mabingwa wa soka Afrika mashariki na kati Azam FC watashuka dimbani mwishoni mwa juma hili kucheza dhidi ya Njombe Mji, katika muendelezo wa mshike mshike wa ligi kuu ya soka Tanzania bara inayoingia kwenye mzunguuko wa 11.

Azam FC wamesafiri hadi mjini Njombe wakitokea Dar es salaam, na watamkosa nahodha na kiungo wao  Himid Mao katika mchezo wa jumapili utakaochezwa kwenye uwanja wa Saba Saba.

Himid ataukosa mchezo huo kufuatia adhabu ya kadi tatu za njano alizoonyeshwa kwenye michezo iliyopita ya ligi kuu.

Wachezaji wengine wa Azam FC watakaokosa mchezo huo wa jumapili ni mabeki kutoka Ghana Daniel Amoah na Yakubu Mohammed ambapo kila mmoja amefikisha kadi tatu za njano.

Kikosi cha Azam kiliwasili mjini Njombe jana saa moja jioni baada ya safari ndefu ya saa 15.

Wachezaji waliowasili na Azam mjini humo ni makipa Razak Abalora, Mwadini Ally na Benedict Haule, mabeki ni Nahodha Msaidizi Aggrey Morris, David Mwantika, Abdallah Kheri, Bruce Kangwa, Hamim Karim na Swaleh Abdallah.

Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Salmin Hoza, Stephan Kingue, Enock Atta Agyei, Ramadhani Singano ‘Messi’, Joseph Mahundi, Idd Kipagwile na washambuliaji ni Mbaraka Yusuph, Waziri Junior, Yahya Zayd na Andrea Simchimba, aliyepandishwa wiki iliyopita kutoka timu ya vijana.

Katika mechi tisa ambazo Azam FC imecheza hadi sasa, imeshinda tano na kutoka sare nne hivyo kujikusanyia pointi 19 sawa na Simba inayoongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao.

Mbwana Samatta aanza mazoezi mepesi
Boti yazama ziwa Victoria ikiwa na watu 17