Conor McGregor ameahidi kumpa kipigo kizito mpinzani wake Khabib Nurmagomedov katika pambano lake la kwanza la MMA/UFC tangu atangaze kurejea kwenye ulingo huo.
Anatarajia kuzichapa na Khabib Jumamosi hii, Las Vegas nchini Marekani katika pambano ambalo linatajwa kuwa kubwa zaidi kwenye historia ya mapigano ya UFC.
McGregor amefunguka alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mkutano wao wa pamoja wa kulitangaza pambano lao.
“Nitampasua, nitamkunja; atapasuka vipandevipande. Sidhani kama ataweza kuvumilia kipigo, atakuwa kama mgeni kwenye UFC,” alisema McGregor.
Mara ya mwisho kwa McGregor kupanda kwenye ulingo wa UFC, ilikuwa Novemba 2016 alipompiga Eddie Alvarez kwenye pambano lao la uzito wa lightweight.
Alivuliwa mataji yote miezi michache baadaye kutokana na kutojihusisha kwa muda mrefu na mapigano hayo.
Hata hivyo, ana kibarua kizito dhidi ya Khabib, mpiganaji kutoka Urusi ambaye hajawahi kupoteza pambano hata moja kati ya mapambano 26, akishinda mapambano yake kwa kuwapa kipigo kikali wapinzani wake.
Khabib pia ameahidi kushinda kwa KO, akisema, “nitamfunga mdomo, atajuta kukubali kupigana na mimi.”