Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi na Watumishi wa Umma kuwajibika kikamilifu katika kutatua kero na changamoto zinazowakabili wananchi.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akizindua Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichopo jijini Mwanza.
Mchengerwa amewakumbusha wafanyakazi wa Serikalini kufanya kazi kwa uadilifu na kutekeleza majukumu yao vema kwani Watanzania wapo zaidi ya milioni 60 na kila mmoja anatamani kufanya kazi Serikalini lakini hawajapata nafasi hiyo.
“Nikiwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ninawaagiza kila mmoja wetu awajibike na kuguswa katika kutatua kero zinazowakabili wananchi,”
Mchengerwa amesisitiza na kuongeza kuwa, Viongozi na Watumishi wa Umma hawawezi kuwa na uhalali wa nafasi zao iwapo hawajishughulishi na kero za wananchi kwani wananchi hao ndio wenye serikali.
Aidha Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inathamini sana wananchi wake, hivyo Viongozi na Watumishi wa Umma kwa nafasi zao waiunge mkono kwa vitendo ili kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.
Akizungumzia mchango wa Serikali katika kuwajali wananchi, Kaimu Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi amesema Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imewanufaisha wananchi 58,000 ambao wamepata ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 61 ambazo zimepokelewa toka Awamu ya Kwanza ya TASAF.
Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 2 na bilioni 300 ambazo zitawezesha kuzifikia kaya zote maskini zenye sifa za kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.