Watanzania watakiwa kubadili mtazamo kwanza badala ya kutaka mabadiliko ya katiba na sheria kabla ya kupima vifungu vilivyopo kama vinatekelezeka na kuleta matokeo bora.

Hayo yamesemwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma baada ya kumwapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Mbuki Feleshi, kuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

“Ningependa kuwaambia watanzania wenzangu, Sheria za Tanzania siyo mbaya, mtazamo ndiyo mbaya. Sheria hii hii ukiipeleka Marekani itafanyakazi vizuri sana. Pengine badala ya kufikiria kufanya mabadiliko ya sheria, tuanze kufikiria mabadiliko ya nafsi. Nafsi zetu zinaheshimu sheria? Nafsi zetu zinafuata utaratibu? Kwa sababu bila sisi wenyewe kufuata utaratibu, hata tukiwa na sheria nzuri namna gani haitasaidia,” amesema Prof. Juma

Prof. Juma amewaambia wananchi uwepo wa utaratibu wa kushughulikia nidhamu katika ngazi ya Majaji, Mahakimu, ambapo kuna ushiriki wa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, viongozi wa dini na wote hao hukaa kushughulikia masuala ya kinidhamu kwa watendaji hao wa Mahakama.

“Ukiangalia sheria inayoendesha shughuli za Mahakama imeunda kamati za maadili. Kuna Kamati za Maadili za Majaji, ambazo zinapokea malalamiko ya kinidhamu dhidi ya Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,”

Aidha amesema kuwa kwa bahati mbaya wananchi wengi hawaelewi uwepo wa utaratibu wa kupokea malalamiko dhidi ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi na Jaji wa Mahakama Kuu na kuna utaratibu wa kumwomba ajileleze mbele ya kamati hiyo na mapendekezo hupelekwa mbele ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na suala hilo likiwa zito hupelekwa kwenye mamlaka ya uteuzi na kuna ngazi zingine za kufanya kama kuna haja ya kumwondoa Jaji kazini.

Jaji Mkuu amewataka wananchi wanapokuwa na malalamiko yanayogusa nidhamu watumie mifumo iliyopo ili kuweze kuipima kama inatosha, na kama haitoshi ifanyiwe marekebisho. “Tusifanye marekebisho bila kupima kama vifiungu vilivyopo vinaweza kufanya kazi,” alisema..

Jaji Mkuu alimwahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali huyo kuwa Mahakama ya Tanzania itaendeleza huo utaratibu aliouweka wa kufuatilia kwa karibu mienendo ya mashauri na kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi yake kwa wakati na hivyo kupunguza malalamiko kwa wananchi.

Rais Samia: mfanye kazi kwa kuzingatia sheria
Mchengerwa:Watumishi wa umma wajibikeni