Mchungaji wa kanisa moja nchini Zimbabwe, Phillip Mugadza ambaye alitabiri kuwa Rais Robert Mugabe atakufa mwezi huu amekwama Mahakamani.
Mahakama Kuu nchini humo imekataa maombi ya Mchungaji Mugadza ya kutaka kesi yake itupiliwe mbali. Jaji Mkuu, Luke Malaba amesema kuwa mchakato wa kesi hiyo unaendelea na kwamba Mahakama hiyo ya juu imerejesha shauri hilo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ambako lilifunguliwa.
Mchungaji huyo ambaye ni kiongozi wa kanisa la Remnant alikamatwa mwezi Januari mwaka huu baada ya kudai amepata maono kuwa Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 93 atafariki dunia Mwezi Oktoba mwaka huu.
Mwanasheria wa mchungaji huyo aliviambia vyombo vya habari kuwa mteja wake amekiri kutoa tamko hilo na kwamba ni kazi ya Polisi kuthibitisha kuwa aliyemwambia sio Mungu.
“Huo ni ujumbe kutoka kwa Mungu. Polisi watatakiwa kuthibitisha kuwa Mungu hakusema hivyo,” BBC inamkariri mwanasheria huyo.
Aliitaka Mahakama kutupilia mbali kesi dhidi ya mteja wake kwa madai kuwa mashtaka dhidi yake yanavunja uhuru wa kuongea.
Mwendesha mashtaka aliiambia Mahakama kuwa Mchungaji huyo aliivunjia heshima dini ya Kikristo na utamaduni wa kiafrika kwa kutabiri kifo cha Rais.
Kwa mujibu wa tamaduni za Kiafrika, ni mwiko kutabiri kifo cha kiongozi.