Wabunge watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Esther Matiko (Tarime Mjini), Esther Bulaya (Bunda Mjini) na Halima Mdee (Kawe) wameachiwa huru kutoka gerezaji baada ya chama hicho kulipa faini ya Sh. 110 Milioni.
Wabunge hao watatu walioachiwa leo, Machi 12, 2020 ni kati ya viongozi wanane wa chama hicho, ikiwa ni pamoja na Dkt. Vincent Mashinji ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho na sasa amehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela au kulipa faini ya Sh 350 Milioni baada ya kukutwa na hatia katika makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.
Hakumu dhidi ya viongozi hao akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ilisomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Viongozi hao walilazimika kwenda jela kwakuwa hawakuwa wamekamilisha taratibu za kulipa faini iliyotakiwa. Hata hivyo, Chadema walianza kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwanusuru viongozi hao na kifungo cha jela, na ndani ya saa 24 walichanga kiasi cha Sh. 234 milioni.
CCM pia ilichanga fedha na jana ilifanikiwa kumtoa gerezaji mfuasi wake, Dkt. Mashinji. Chama hicho kilimlipia Sh. 30 milioni.
Akizungumza baada ya kutoka jela, Mdee amewashukuru Watanzania kwa kuwachangia fedha za kulipia faini akidai kuwa hawakuwa na fedha za kulipa faini hiyo.
“Nawashukuru Watanzania, walijua hatuna fedha, ni kweli hatukuwa na pesa kabisa, walijua mapema tunaenda jela,” alisema Mdee aliyekuwa akitoa machozi na kuongeza kuwa akaunti za Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe zimefungwa.