Aliyekua Mshambuliaji wa Simba SC Meddie Kagere amewashukuru Viongozi, Wachezaji, Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kwa kumuonesha upendo na kumuaga kwa heshima katika tukio maalum wakati wa Tamasha la Simba Day jana Jumatatu (Agosti 08).
Kegere na Kiungo kutoka nchini Uganda Thadeo Lwanga walipata nafasi ya kipekee kuagwa na Mashabiki wa klabu ya Simba SC Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku wakitoa neno la shukurani mbele ya umma uliokua umejitokeza Uwanjani hapo.
Baada ya kukamilisha taratibu wa kuagwa, Mshambuliaji huyo kutoka nchini Rwanda aliendelea kutoa shukurani nyingine kwa Viongozi, Wachezaji na Mashabiki wa Simba SC kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Kagere aliyejiunga na Singida Big Stars saa chache baada ya kutangazwa hatokua sehemu ya Simba SC juma lililopita ameandika: “Nilikuja kama Mfalme na sasa naondoka kama Gwji, Ahsanteni Mashabiki wote wa Simba kwa upendo wenu, Heshima kwa wachezaji wenzangu na Mashabiki kwa kuwa sehemu ya safari yangu.”
Meddie Kagere alisajiliwa Simba SC msimu wa 2017/18 akitokea Gor Mahia ya Kenya na amekua sehemu ya mafanikio ya Klabu hiyo ya Msimbazi kwa miaka minne mfululizo, huku akiibuka kinara wa kupachika mabao mara mbili mfululizo katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.