Siku kuu ya Wafanyakazi hufanyika Mei mosi ya kila mwaka kwa wafanyakazi hupata fursa ya kuwasilisha changamoto zao kwa mwajiri ili ziweze kupata ufumbuzi ikiwemo suala la upandaji wa madaraja na ongezeko la Mishahara ambapo safari hii Serikali imeahidi kufanya mambo kimyakimya.
Katika maadhimisho ya siku hiyo hii leo Mei Mosi, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, kujitoa kwa wafanyakazi na bidii walizonazo zinasaidia kujenga Taifa na kwamba kazi kubwa waliyonayo inaleta hamasa ya uwajibikaji na matokeo chanya.
Amesema, “Ndugu zangu wafanyakazi kile watu walichozoea tukiseme hapa ili wapandishe bei madukani mara hii hakuna tunakwenda kufanya mambo polepole, wasione tumeongezeana kitu gani ili mwenendo wetu wa bei uwe salama.”
Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa, “Kuna nyongeza za mishahara za kila mwaka ambazo zilisitishwa kwa muda, nikaona mwaka huu nizirudishe, nyongeza hizo za kila mwaka zitaanza mwaka huu na zitaendelea kila mwaka.”
Hata hivyo ameongeza kuwa, mbali na upandishaji wa posho, mwaka huu pia Serikali itaendelea kupandisha madaraja, vyeo na madaraja na kwamba ilipotoa nyongeza za posho, bajeti ilikuwa ishapita, hivyo mavuno ya posho hizo yatakuja kwenye bajeti ya mwaka huu.